UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI DAR ES SALAAM WAANZA RASMI NI SULUHU YA KUDUMU YA MAFURIKO
Dar es Salaam,
21/07/2025
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza rasmi ujenzi wa daraja jipya la kisasa katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudumu wa kuondoa changamoto ya mafuriko ya mara kwa mara yanayoathiri jiji hilo.
Daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 390, na linajengwa kwa viwango vya juu vya kisasa ili kuhakikisha uimara na usalama wa muda mrefu, ambapo kwa mujibu wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, tayari mkandarasi wa mradi amepokea malipo ya awali na ujenzi umeanza kwa kutengeneza barabara ya muda (diversion) itakayotumika kupitisha magari wakati wa ujenzi.
"Daraja hili ni la kimkakati, linalenga sio tu kupunguza madhara ya mafuriko bali pia kuboresha usafiri katika eneo hili muhimu, ujenzi huu unahusisha pia njia za maingilio na barabara za magari pamoja na njia salama za watembea kwa miguu," alisema Mha. Kyamba.
Ameongeza kuwa mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es Salaam na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na foleni za magari.
Daraja la Jangwani ambalo lipo kwenye barabara ya Morogoro linalotarajiwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa, litachangia kuimarisha mfumo wa usafiri kutoka katikati ya jiji na maeneo ya Ilala, Buguruni, pamoja na sehemu nyingine zinazotegemea barabara ya Morogoro.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa mradi huu na kuuwezesha kuanza. Wananchi wamekuwa wakingoja kwa muda mrefu kuona suluhisho la kudumu kwa tatizo la mafuriko ambalo limekuwa likisumbua kwa miaka mingi,” aliongeza Mha. Kyamba.
Mradi huu ni sehemu ya miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa jijini Dar es Salaam chini ya usimamizi wa TANROADS, ikiwemo uboreshaji wa barabara kuu na madaraja muhimu kwa maendeleo ya jiji.