MWENGE WA UHURU WATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA DARAJA HANANG’
Hanang’
18/07/2025
Mwenge wa Uhuru umetembelea mradi wa ujenzi wa daraja katika Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, mradi unaotekelezwa katika barabara ya Gehandu–Babati, eneo la Katesh.
Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, huku msafara wa Mwenge wa Uhuru ukiongozwa Kiongozi wake wa Kitaifa Bw. Ismail Ali Ussi na kupokelewa na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara, Mhandisi Dutu Masele.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mha. Masele alisema ujenzi wa daraja hilo umetokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu uliosababishwa na maafa yaliyotokea mwaka 2023 katika wilaya hiyo.
“Mradi huu utaenda kuzuia athari ambazo zinaweza kujitokeza. Daraja hili lina uwezo wa kupitisha maji bila shida yoyote,” alisema Mha. Masele.
Aidha, alimhakikishia Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kasi na utamalizika kwa wakati kama ilivyopangwa, huku wahandisi wa TANROADS wakiendelea na kazi kuhakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa. Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Rotronic Ltd.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Bw Ussi aliwapongeza TANROADS kwa kusimamia mradi huo kwa ufanisi mkubwa na kufanikisha hatua ya ujenzi iliyofikiwa. Pia alitoa pongezi kwa wahandisi wa TANROADS kwa umahiri na umakini waliouonesha katika utekelezaji wa kazi hiyo.