Dar es salaam
17/07/2025
MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA: DAR ES SALAAM YAPATA UVUMBUZI MKUBWA WA MIUNDOMBINU
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jiji la Dar es Salaam limepata mageuzi makubwa ya miundombinu, yakijidhihirisha kupitia ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja muhimu.
Katika kukabiliana na athari za mvua kali za El-Nino zilizoharibu miundombinu ya jiji, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 61 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa barabara na madaraja yaliyoharibiwa. Miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea ni pamoja na:
- Daraja la Mkwajuni (sh. bilioni 11.6)
- Daraja la Kigogo lenye urefu wa mita 50 (sh. bilioni 17)
- Daraja la Mtongani, Amani Mbovu, Geti Jeusi, na Kisarawe
Kwa mujibu wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, ujenzi wa daraja la Jangwani lenye urefu wa mita 390 tayari umeanza. Mkandarasi amelipwa na tayari ametengeneza njia mbadala ili kuruhusu ujenzi kuendelea bila vikwazo.
Aidha, mradi wa upanuzi wa awamu ya kwanza ya barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kutoka Ubungo hadi Kimara umefikia asilimia 52, na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu. Mradi huu utapunguza msongamano mkubwa wa magari na kuongeza ufanisi wa usafiri wa umma.
Katika hatua nyingine, barabara ya Mbagala Rangi Tatu–Kongowe itapanuliwa kuwa njia nne, ikiwa ni maandalizi ya huduma za mwendokasi na kupunguza msongamano katika eneo hilo.
Kwa sasa, Dar es Salaam ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 619.01, nyingi zikiwa ni njia nne hadi nane. Serikali inaendelea kuboresha mtandao huo kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati.
Kitengo cha Maabara cha TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam pia kinahusika kuhakikisha ubora wa miradi hiyo kwa kufanya vipimo vya kitaalam katika barabara na madaraja yote yanayojengwa.
Serikali imeendelea kushirikiana na wakandarasi wazawa katika kutekeleza miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara za Kimara–Bonyokwa na Kibada–Mwasonga hadi Kimbiji, hatua inayotoa ajira kwa Watanzania na kukuza ujuzi wa ndani.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kyamba, miradi yote ya dharura ya shilingi bilioni 61 inatekelezwa na wakandarasi wa ndani, isipokuwa daraja la Mtongani.
Mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kujenga jiji la kisasa lenye miundombinu thabiti, salama na ya kuaminika – inayowezesha shughuli za kiuchumi, kijamii na usafirishaji kukua kwa kasi zaidi.