News

MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA LIKUYUFUSI-MKENDA WAZINDULIWA RASMI MKOANI RUVUMA

MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA LIKUYUFUSI-MKENDA WAZINDULIWA RASMI MKOANI RUVUMA

22 Juni, 2025

Ruvuma

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imezindua rasmi mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Likuyufusi–Mkenda, sehemu ya Likuyufusi–Mkayukayu yenye urefu wa kilomita 60, hafla iliyofanyika katika Kijiji cha Litapwasi, Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Ferdinand Mdoe, alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuunganisha mikoa ya ndani na nchi jirani kupitia miundombinu bora ya barabara.

“Barabara hii ni kiunganishi muhimu kati ya Wilaya ya Songea na Nyasa, pamoja na nchi jirani ya Msumbiji kupitia daraja la Mitomoni,” alisema Mdoe.

Kwa mujibu wa Mha. Mdoe, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara yote yenye urefu wa kilomita 124, na kugawanya ujenzi wake kwa awamu.

Mradi huu wa sasa unajengwa na kampuni ya China First Highway Engineering Co. Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 110.77, ukitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 27.

Aidha, maandalizi ya ujenzi yameshaanza, ambapo mkandarasi yupo katika hatua ya kukamilisha taratibu za dhamana za benki ili kuanza rasmi kazi.

Mkataba wa ujenzi ulisainiwa tarehe 10 Juni 2025.Mha. Mdoe alibainisha kuwa fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo tayari imefanyiwa tathmini, ambapo waathirika 851 wametambuliwa na wanatarajiwa kulipwa fidia ya Shilingi Bilioni 5.195.

Malipo hayo yatafanyika mapema kabla ya kuanza kwa kazi za ujenzi.Wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi huo wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazotokana na utekelezaji wa ujenzi huo, ikiwemo ajira, biashara na mafunzo ya ujuzi.

TANROADS pia imetoa wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na mkandarasi, hususan katika ulinzi na utunzaji wa vifaa vya ujenzi.

Serikali pia imepanga kuendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa sehemu ya Mkayukayu – Mkenda (Km 64) pamoja na kukamilisha ujenzi wa madaraja ya kudumu ya Mitomoni na Mkenda, ili kuhakikisha barabara yote ya Likuyufusi–Mkenda inakuwa ya kiwango cha lami.

Kukamilika kwa mradi huu kutarahisisha usafiri kati ya Songea na Nyasa, na kufungua fursa za kibiashara na kijamii kati ya Tanzania na Msumbiji.