News

MTENDAJI MKUU TANROADS AKAGUA UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA, WAFIKIA ASILIMIA 70

MTENDAJI MKUU TANROADS AKAGUA UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA, WAFIKIA ASILIMIA 70

Sumbawanga

21 Juni, 2025

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, leo Jumamosi Juni 21, 2025 ametembelea kiwanja  cha ndege cha Sumbawanga, kukagua maendeleo ya ujenzi wake ambao unaendelea kwa kasi.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mha. Besta amesema ujenzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 70, ambapo sehemu ya kuruka na kutua ndege (runway) tayari imekamilika, na kazi imebakia kwenye mita 15 kati ya kilometa 1.7.

Ameongeza kuwa, baada ya kukamilisha sehemu hiyo, mkandarasi ataanza kazi ya kuweka alama (markings) kwenye barabara ya kutua na kuruka ndege, barabara za kuingilia ndege (taxiways), maegesho ya ndege (apron), pamoja na kuweka taa maalum (flight lights) kwa ajili ya usiku.

“Nimeridhishwa na maendeleo ya kazi hii na napenda kumpongeza msimamizi kutoka kampuni ya SMEC International kwa kusimamia kwa umakini na kuhakikisha kazi zinaendelea vizuri. Natarajia uwanja huu utakuwa tayari kutumika kuanzia mwezi Julai hadi Agosti,” alisema Mha. Besta.

Aidha, amemuelekeza mkandarasi kutoka kampuni ya BCEG pamoja na msimamizi SMEC International kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kuweka alama za usalama kwa mujibu wa viwango na kuzingatia kanuni.

Kiwanja cha ndege cha Sumbawanga kinatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa mkoa wa Rukwa kwa kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga na kuufungua kiuchumi.