MAJALIWA AKOSHWA DHAMIRA YA RAIS SAMIA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI MIRADI
Mwanza
19 Juni, 2025
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha kutekeleza na kukamilisha miradi mingi ya kimaendeleo nchini.
Majaliwa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa daraja la J.P Magufuli lililozinduliwa rasmi leo Juni 19, 2025 jijini Mwanza na Rais Samia, huku akiwaambia wananchi kuwa Rais Samia ana mapenzi mema na nchi ya Tanzania.
"Mwenyezi Mungu hamuachi mtu mwenye mapenzi mema kwa Watu wake, wewe (Rais Samia) una mapenzi mema kwa Watanzania na maelekezo yako kwa wasaidizi wako nikiwemo mimi tunaendelea kusimamia maelekezo yako," amesema Majaliwa.
“…Mheshimiwa Rais endelea na kazi chapa kazi, Mwenyezi Mungu atakujalia, atakuongoza, atakuondoshea wabaya wote ili ufanye kazi yako vizuri,” amesema Majaliwa.
Daraja hilo limezinduliwa leo na Rais Samia baada ya kukamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh.700 Bilioni.