DARAJA LA J.P MAGUFULI LITAISHI ZAIDI YA MIAKA 100
Mwanza
19 Juni, 2025
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta amesema usanifu uliofanywa na makisio yake kwa daraja la J.P Magufuli ni kwamba daraja hilo litaishi zaidi ya miaka 100.
“Katika usanifu tulifanya makisio ya kitaalamu kwamba daraja hili lidumu sio chini ya miaka 100, na baada ya daraja hili kuzinduliwa na kuanza kutumika na magari kumekuwa na mpango maalumu wa usimamizi wa matengenezo (maintanance program) ya daraja hili utakaosimamiwa na TANROADS wenyewe,” amesema Mha. Besta na kuongeza kuwa
… “Daraja hili ni gumu kulijenga na gumu vilevile kulisimamia, hivyo lazima tuwe na mpango maalumu wa usimamizi wa matengenezo ili kuendelea kulitathmini linavyoendelea kutoa huduma kwa magari na wananchi ili kuhakikisha linadumu kwa miaka tuliyopanga.
Hili linafanyika kwa hadi daraja la Dar es Salaam la Tanzanite.”Mha. Besta ameyasema hayo leo Juni 19, 2025 wakati wa mahojiano kwenye Kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1, kabla ya uzinduzi rasmi wa daraja hilo uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hii leo.