News

MATUMIZI YA KIJAMII NA KITALII DARAJA LA KIGONGO-BUSISI KULIPIWA BAADA YA RIDHAA YA MHE. RAIS

MATUMIZI YA KIJAMII NA KITALII DARAJA LA KIGONGO-BUSISI KULIPIWA BAADA YA RIDHAA YA MHE. RAIS

Mwanza

08 Juni, 2025

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega (MB), amesema kuwa matumizi ya kijamii na ya kitalii ya Daraja la Kigongo–Busisi, ikiwemo harusi, kurekodi nyimbo pamoja na utaratibu wa malipo kwa magari ya kibiashara, yatategemea kibali maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza terehe 08 Juni, 2025 katika hafla ya kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya wizara hiyo ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Waziri Ulega amesema baadhi ya wananchi tayari wameonyesha nia ya kulitumia daraja hilo kwa shughuli mbalimbali, lakini kabla ya vibali kutolewa, lazima kwanza ipatikane ridhaa ya Rais.

“Matumizi mengine ikiwa ni ya utalii na watani zangu Wasukuma wanaweza kutaka kuja kufanya harusi zao, kurekodi kwaya, kaswida na mambo mengine ya kijamii, kimsingi sisi tumekasimiwa mamlaka na Mheshimiwa Rais, kwa hiyo mimi ninayo kazi ya kumuomba na kumjulisha kwamba wapo Watanzania wanaotaka kuja kufanya mpaka picha za harusi hapa.

“Kabla ya kutoa vibali, tutamshirikisha Rais, na tukipewa kibali sisi maana yake tutatumia njia ya kuwaambia Watanzania wote kuhusu utaratibu maalum kwa ajili ya usalama wa watu, watumiaji hao, kwa sababu hapa malori yatakuwa yanapita tena kwa kasi.”

Tumeshaanza kupokea maoni mfano kutoka kwa baadhi ya wabunge wanasema wananchi wasilipishwe lakini malori ya biashara lazima yachangie kwa sababu hapa panahitajika maintanance, lakini jambo hili halijafika mwisho, linahitaji mjadala na linahitaji kuridhiwa na litakaporidhiwa tutatangaza hadharani. amesema Ulega