News

MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA MADARAKANI VIWANJA 12 VYA NDEGE VYABORESHWA NA SASA UJENZI MSALATO WASHIKA KASI

MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA MADARAKANI VIWANJA 12 VYA NDEGE VYABORESHWA NA SASA UJENZI MSALATO WASHIKA KASI

Mwanza

08 Juni, 2025

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kusukuma mbele juhudi za kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga kwa kasi na mafanikio makubwa.

Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, amesema hayo Juni 08, 2025 jijini Mwanza alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini, ikiwepo mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, ambacho kipo katika hatua ya juu ya utekelezaji.

"Ujenzi sehemu ya kwanza ikihusisha njia ya kuruka na kutua ndege (runway) na miundombinu mingine imefikia asilimia 87, huku ujenzi wa jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege na miundombinu mingine yote umefikia asilimia 53," alisema Waziri Ulega.

Mbali na Msalato, Serikali pia inaendelea na maboresho ya viwanja vingine vya ndege katika mikoa mbalimbali ikiwemo Kigoma, Tabora, Geita, Songwe, Mtwara, Sumbawanga, Iringa, Musoma, Shinyanga, Songea, Tanga na Lake Manyara.

Maboresho ya viwanja vingi kati ya hivyo vimeshakamilika, na hatua hiyo inaelezwa kuwa ni kielelezo cha dhamira ya Serikali kuimarisha usafiri wa anga kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Waziri Ulega amesisitiza kuwa miradi hii ni ya kimkakati na itaongeza ufanisi wa usafiri wa abiria, biashara na utalii, sambamba na kufungua fursa zaidi kwa wananchi wa maeneo husika.