RC CHONGOLO AKAGUA UJENZI WA DARAJA LA KAMSAMBA, APONGEZA USIMAMIZI WA TANROADS
Songwe,
06 Juni, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Mpapa-Kakonko maarufu kama Daraja la Kamsamba lililopo katika Wilaya ya Momba, akisisitiza dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu ya usafiri na mawasiliano.
Katika ziara hiyo, RC Chongolo aliambatana na wataalamu kutoka ofisi yake pamoja na timu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Songwe ikiongozwa na Meneja wa mkoa huo, Mhandisi Suleiman Bishanga.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mhandisi Bishanga alisema kuwa ujenzi wa daraja hilo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 7, ambapo kampuni ya Abemulo Contractors Co. Ltd ndiyo inatekeleza mradi huo kwa mkataba wa miezi 12 hadi kukamilika kwake.
RC Chongolo ameipongeza TANROADS kwa usimamizi madhubuti wa mradi huo muhimu kwa wananchi wa Momba na maeneo jirani, akibainisha kuwa daraja hilo ni mkombozi kwa uchumi wa wakazi wa eneo hilo hasa katika msimu wa mvua ambapo mawasiliano hukatika.
“Nawapongeza TANROADS kwa kazi nzuri mnayofanya, lakini pia nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizi za miradi ya kimkakati zinazogusa maisha ya wananchi wa kawaida,” alisema Chongolo.
Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu bora ya barabara vijijini na mijini, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii