News

TANROADS KUKIJANISHA JIJI LA DODOMA KWA KUPANDA MITI 150,000

TANROADS KUKIJANISHA JIJI LA DODOMA KWA KUPANDA MITI 150,000 Dodoma 05 Juni, 2025 Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na zoezi la kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kijani kwa kupanda miti 150,000 kwenye barabara nne za mzunguko wa nje kupitia mradi wa Kijanisha Jiji la Dodoma (Green Solution Project - GSP), unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Mratibu wa mradi huo kutoka TANROADS, Bw. Julius Luhuro, amesema kuwa mradi huu wa upandaji miti ni wa kimkakati na umelenga kulisaidia Jiji la Dodoma kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Ameeleza kuwa mradi huu unasimamiwa na TANROADS kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). "Lengo kuu la mradi huu ni kuongeza uwezo wa Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi," alisema Bw. Luhuro. Ameongeza kuwa zoezi hilo linatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na linaendeshwa na Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kambi ya Makutupora. “Barabara hii itakuwa ya mfano kwa kuwa na ukanda wa kijani kutokana na miti itakayopandwa, na hivyo kusaidia kupunguza gesi joto kwa kuongeza uoto wa asili,” alieleza. Hadi kufikia sasa, miti 35,000 imekwishapandwa katika maeneo ya barabara ya mzunguko wa nje ya Jiji la Dodoma, yenye urefu wa kilomita 112, tangu kuanza kwa zoezi hilo mwezi Novemba 2024. Kuhusu changamoto ya ukame, Bw. Luhuro amesema kuwa visima 11 tayari vimechimbwa kwa ajili ya umwagiliaji wa miti hiyo, ambapo teknolojia ya umwagiliaji wa matone ndiyo itatumika kuhifadhi maji. Kwa upande wake, Meneja wa Mazingira na Usimamizi wa Kijamii wa TANROADS, Bi. Zafarani Madayi, amesema taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza zoezi endelevu la upandaji miti katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara kwa lengo la kuboresha mazingira. Aidha, Bi. Madayi ametoa wito kwa wananchi kuacha kutupa taka za plastiki ovyo, hasa kwenye mifereji, kwani ni chanzo kikuu cha kuziba kwa mifereji hiyo wakati wa mvua na kuharibu barabara.