News

TANROADS YATUNUKIWA TUZO KWA MCHANGO WAKE WA KUPUNGUZA GESIJOTO NCHINI

TANROADS YATUNUKIWA TUZO KWA MCHANGO WAKE WA KUPUNGUZA GESIJOTO NCHINI

 Dodoma

06 Juni, 2025

Katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu, Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ilitunukiwa tuzo maalum kwa kutambua mchango wake mkubwa katika juhudi za kitaifa za kukabiliana na ongezeko la gesi joto nchini. Tuzo hiyo ilitolewa Tarehe 5 Juni 2025 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan TANROADS ilipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, ikiwa ni kutambua kazi nzuri na jitihada endelevu katika kulinda mazingira na kutekeleza miradi rafiki kwa tabianchi. Akizungumza kwa niaba ya TANROADS, Zafarani Madayi ambaye ni Meneja wa Mazingira na Usimamizi wa Kijamii, alisema kuwa tuzo hiyo ni matokeo ya jitihada za pamoja kati ya TANROADS na Wizara ya Ujenzi katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa kuzingatia uendelevu wa mazingira. “Katika miradi yetu mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), tumeweza kufikia mafanikio makubwa. Hadi sasa, tumeendelea na utekelezaji wa awamu ya kwanza hadi ya nne, na maandalizi ya awamu ya tano yamefikia hatua nzuri,” alisema Madayi. Ameongeza kuwa mbali na miradi hiyo, TANROADS imekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti kwa wingi kote nchini. Mwaka huu pekee, TANROADS imefanikiwa kupanda miti takribani 68,000, ikiwa ni mafanikio makubwa ukilinganisha na lengo la miti 40,000 walilojiwekea mwaka jana. Katika Jiji la Dodoma pekee, zaidi ya miti 40,000 imepandwa, hususan kandokando mwa barabara ya mzunguko (Dodoma Outer Ring Road), kupitia Mradi wa Green Solution (Kukijanisha Jiji la Dodoma) unaotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB). “Tuzo hii tumeipokea kwa furaha kubwa sana TANROADS. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wetu na kutupatia tuzo hii ya heshima. Pia tunatoa shukrani zetu kwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutuweka miongoni mwa taasisi zenye mchango mkubwa katika juhudi za serikali za kupunguza gesi joto nchini,” aliongeza Madayi.