Daraja lililojengwa katika eneo la Morena kuelekea Chimwaga (Morena-Chimwaga JCT Round about) jijini Dodoma limekamilika na sasa limefunguliwa kwa matumizi ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Elisony Mweladzi, ameseama kukamilika kwa daraja hilo ni hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto ya mafuriko yaliyokua yakisababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo, hasa wakati wa mvua.
"Tunapenda kuwataarifu rasmi kuwa barabara hii sasa imefunguliwa na daraja limekamilika kwa viwango bora. Wananchi waendelee kulitumia, "amesema Mhandisi Mweladzi.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imefanikiwa kulitatua tatizo hilo kwa msaada wa fedha kutoka kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan, ambaye ameelezwa kuwa mhimili mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya Miradi ya maendeleo.
Mradi huo wa ujenzi wa daraja umetekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia(World Bank) na mkandarasi M/S Andic Limited, kwa gharama ya shillingi Billioni 1.5.
Kwa upande wake, Mhandisi Andrew Kaywanga kutoka kampuni ya Andic Limited ameseama mradi huo uliopaswa kukamilika ndani ya mwaka mmoja, umemalizika kwa miezi mitano na nusu tu, kutokana na kazi ya usiku na mchana iliyofanywa ili kuharakisha ukamilishaji wake.
"Tumejitaidi kuhakikisha tunamaliza mapema ili kuepusha usumbufu kwa wananchi waliokua wakitegemea njia hii muhimu", amesema mhandisi Kaywanga.
Aidha,ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa menejimenti ya TANROADS Mkoa wa Dodoma na Wizara ya Ujenzi kwa ushirikiano wao mkubwa uliofanikisha mradi huo.
Naye mkazi wa kijiji cha Chaduru, Emilian Makola, ameishukuru serikali kwa kukamilisha daraja hilo ambalo sasa limeondoa adha ya mzunguko mkubwa waliokuwa wakiupitia wakati wa mvua.
"Daraja hili sasa litatusaidia sana kuepuka mafuriko na kufupisha safari, tunatoa shukrani zetu kwa serikali, "amesema Makola.