News

BARABARA YA KUTUA NDEGE UWANJA WA MSALATO KUFUATA  VIWANGO VYA ICAO

BARABARA YA KUTUA NDEGE UWANJA WA MSALATO KUFUATA  VIWANGO VYA ICAO

 

Dodoma

27 Mei, 2025

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amefanya ukaguzi wa maendeleo ya kazi ya ujenzi katika Uwanja wa Ndege wa Msalato, ambapo kwa sasa kazi ya kuweka alama kwenye njia ya kurukia na kutua ndege (runway) inaendelea kwa kasi.Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 27,2025 jijini Dodoma, Mhandisi Besta amesema kuwa ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu wa kilomita 3.6 na upana wa mita 60 umekamilika kwa kiwango cha kuwekwa tabaka la mwisho la lami. Kazi inayoendelea sasa ni uwekaji wa alama za kuongozea ndege, na inatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 30, 2025.“Zoezi hili linafanyika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vinavyotolewa na Shirika la Anga la Kimataifa (ICAO), kupitia ambatanisho la 14, tunahakikisha kuwa kila hatua inafuata taratibu na miongozo ya kimataifa kwa ajili ya usalama na ufanisi wa uwanja huu,” amesema Mha. Besta.

 

Aidha, ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa uwekaji wa alama, hatua inayofuata itakuwa ni ufungaji wa mfumo wa taa za kumwongoza rubani, ili kuruhusu matumizi ya uwanja huo nyakati zote, ikiwemo usiku.Amesema vifaa vya taa pamoja na mifumo ya umeme tayari vimewasili na maandalizi ya kuviweka yameanza.“Taa hizi zitasaidia kuwaongoza marubani wakati wa kuruka na kutua, hivyo kuongeza usalama wa safari za anga, mfumo huu ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha uwanja huu unafanya kazi kwa ufanisi mkubwa,” aliongeza.

 

Halikadhalika, Mha. Besta amesema kuwa TANROADS imekamilisha ukaguzi wa awali wa kiufundi na taarifa zimekusanywa ili kuwezesha TCAA (Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania) kuingiza taarifa za uwanja wa Msalato katika machapisho yao rasmi, hatua itakayosaidia umma na mashirika ya anga kuutambua rasmi uwanja huo.Akihitimisha, amesema kuwa kwa sasa kazi ya ujenzi wa njia ya kuruka na kutua kwa ndege imefikia asilimia 89 ya ukamilikaji na matarajio ni kuwa uwanja huo utakamilika kwa wakati na kuanza kutumika kwa shughuli mbalimbali za usafiri wa anga.