WATUMISHI WA TANROADS MKOA WA DODOMA WAPATIWA ELIMU YA UGONJWA WA AFYA YA AKILI
Dodoma
23 Mei, 2025
Watumishi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma leo Mei 23, 2025 wameshiriki mafunzo maalum ya afya ya akili yaliyoandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiafya zinazohusiana na msongo wa mawazo.
Mafunzo hayo yametolewa na mtaalamu wa afya ya akili, Dkt. Garvin Kweka, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika afya ya akili kwa watumishi wa umma.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Kweka amebainisha kuwa afya ya akili imekuwa moja ya changamoto kubwa inayoathiri utendaji kazi wa watumishi wengi katika maeneo mbalimbali.
Amesisitiza kuwa kukabiliana na tatizo hili kunahitaji mbinu za msingi ambazo kila mtu anaweza kujifunza na kuzitekeleza katika maisha ya kila siku.
Vilevile ameeleza kuwa njia kuu tatu ambazo zinaweza kusaidia kuondoa tatizo hili ni kuweza kudhibiti hisia, fikra, na tabia.
“Tukifanikiwa haya mambo makubwa matatu basi tutakuwa tumefanikiwa kupambana na tatizo la afya ya akili,” ameeleza Dkt. Kweka, huku akihamasisha watumishi hao kujijengea tabia ya kujitambua na kutafuta msaada mapema pindi wanapohisi mabadiliko katika afya ya akili.
Mafunzo hayo yametajwa kuwa sehemu ya mikakati ya kuboresha ustawi wa watumishi na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi serikalini.