News

BARABARA  NJIA NNE IGAWA-TUNDUMA KM 218 KUJENGWA  KWA AWAMU

BARABARA  NJIA NNE IGAWA-TUNDUMA KM 218 KUJENGWA  KWA AWAMU

 

Dodoma

14/05/2025

Serikali inaendelea kutekeleza  Ujenzi wa barabara ya njia nne kwa awamu kuanzia  Igawa - Uyole - Songwe hadi Tunduma yenye urefu wa kilometa 218 kwa  kiwango cha lami.

 

Hayo yameelezwa leo Mei 14, 2025 Bungeni  jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Juliana Shonza aliyeuliza ni lini, ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma utaanza.

 

“Serikali inaendelea na utekelezaji wa barabara hii ambapo imeanza na upanuzi sehemu ya Nsalaga-Ifisi hadi Songwe KM 36 na kwa sasa ujenzi huu umefikia asilimia 25, aidha Serikali inaendelea na maandalizi ya kuijenga sehemu ya barabara iliyobaki kwa utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi yaani PPP”- amesema Mha. Kasekenya.

 

Aidha, Mha. Kasekenya amesema Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya fidia kwa wananchi  waliopisha barabara  ya bypasi ya Uyole-Songwe na taratibu za kuwalipa zinafanyika

 

"Mhe. Naibu Spika Barabara hiyo imetengewa Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2025/26  na mwaka ujao  wa fedha 2026/27 pia tumeshapata Mkandarasi na tupo katika hatua za mwisho kabisa ili aweze kuanza  kazi katika  sehemu za barabara  hiyo ambazo ni barabara ya Kamsamba- Mlowo na Mbalizi-Mkwajuni ili  kupunguza msongamano mkubwa wa magari  mpakani mwa Tanzania na Zambia",- amesisitiza Naibu Waziri.

 

Katika hatua nyingine, Mha. Kasekenya ameeleza kuwa Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa madaraja ya mto Chobe, Yusa na Nkoma yaliyopo katika barabara ya Mwangongo-Lalago-Meatu mto Sibiti  Km 20.78, ambapo inatafuta fedha kwa ajili ya madaraja hayo.