ULEGA AMUONYA VIKALI MKANDARASI WA CHINA RAILWAY
Tanga,
12/05/2025
Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amempunguzia Kazi ya ujenzi Mkandarasi China Railway 15 Bureau Group anayetekeleza Ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani- Mkwaja- Bagamoyo na kumlipisha faini kutokana na uzembe katika ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Kulingana na Waziri Ulega aliyekagua ujenzi wa barabara hiyo na barabara ya Tungamaa- Mkwaja-Mkange leo Mei 12, 2025, ameeleza kuwa Mkandarasi huyo sasa atatekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa Kilomita 70 pekee kutoka 95.2 alizokuwa amekabidhiwa awali na tenda itatangazwa kumpata Mkandarasi atakayetekeleza kipande cha barabara kilichosalia.
"Huyu Mkandarasi ni miongoni mwa makandarasi wazembe tulionao. Hatudai hata senti kumi, tumemlipa Bilioni 47, Kipande chake cha barabara kilikuwa Km 95.2 azijenge kwa kiwango cha lami na ndani yake kulikuwa na madaraja na Makalavati kadhaa. Tumempunguzia kazi, tumemtoa katika Km 95 tumemshusha mpaka Km 70 na tumempa mpaka Mwezi wa 10 awe kazi yote ameikamilisha." Amesema Waziri Ulega.
Aidha akizungumzia kipande kingine cha barabara hiyo, Waziri Ulega amebainisha kuwa kipande cha Tanga- Pangani-Pangani- Kigombe, kufikia mwezi Juni itakuwa imekamilika huku Mkandarasi akitafutwa kwaajili ya Ujenzi wa Kilomita 70 za Mkange-Bagamoyo na Kilomita 25 zilizoondolewa kwa China Railway 15 Bureau Group.
Aidha akijibu maombi ya Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani Jumaa Aweso, Waziri Ulega ameagiza kukarabatiwa kwa barabara ya Kipungwe-bandarini ili iweze kupitika muda wote pamoja na kufungwa kwa taa kwenye eneo hilo ili kuruhusu shughuli za kiuchumi kufanyika muda wote.
Awali Waziri Ulega alitoa pole pia kwa Waziri Aweso na familia yake kwa ujumla kufuatia kifo cha mdogo wake kilichotokea juma lililopita.