DARAJA LA J.P MAGUFULI KUONGEZA UCHUMI WA TAIFA-ULEGA
Dodoma
05 Mei, 2025
WAZIRI wa Ujenzi, Albdallah Ulega amesema mradi wa kielelezo wa ujenzi wa Daraja la Magufuli lililopo Kigongo- Busisi mkoani Mwanza unatarajiwa kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na nchi jirani.Pia amesema daraja hilo limekamilika kwa asilimia 99 na kulieleza Bunge kuwa matarajio ni kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wake unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.Ulega ameeleza hayo leo Mei 05,2025 bungeni Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2025/26, akieleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa faraja kubwa kwa wakazi wa Kanda ya ziwa ambao wamekuwa wakitumia muda wa takribani saa mbili kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine."Baada ya daraja hili kukamilila muda wa kuvuka unatarajiwa kupungua kufikia wastani wa dakika tatu, aidha daraja hili linategemewa kuongeza shughuli za kiuchumi ndani na nje ya Mikoa ya kanda ya ziwa na nchi jirani lakini pia daraja hili litamywa mojawapo ya alama na fahari ya taifa letu kwani kwa urefu wake wa Kilomita 3.2 litakuwa daraja refu zaidi katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na kati," Ameeleza Ulega.Katika hatua nyingine Ulega ameeleza kuwa mara baada ya kuzinduliwa kwa daraja hilo na kuanza kutumika kikamilifu, vivuko vyote vilivyokuwa vinatumika kwenye eneo hilo la Kigongo-Busisi vitapelekwa katika maeneo mengine nchini yatakayokuwa na uhitaji wa huduma hiyo.Ulega amemshukuru na kutoa pongezi kwa Rais Samia ambaye si tu amelipa gharama zote kwa wakati kwa mkandarasi wa ujenzi huo lakini pia amekamilisha mradi huo ambao ulikuwa ni ndoto ya Mtangulizi wake Hayati Dk John Pombe Magufuli.