News

SERIKALI IMEANZA UBORESHAJI BARABARA YA KIRANJERANJE-NANJIRINJI-RUANGWA

SERIKALI IMEANZA UBORESHAJI BARABARA YA KIRANJERANJE-NANJIRINJI-RUANGWA

 

Dodoma

15 April, 2025

Serikali imeeleza kuwa imeanza utekelezaji wa barabara ya Kiranjeranje-Nanjirinji hadi Ruangwa kwa kuanza na ujenzi wa madaraja makubwa matatu yaliyopo katika barabara hiyo yenye jumla ya urefu wa kilometa 120 Mkoani Lindi.

 

Hayo yameelezwa jijini Dodoma leo Aprili 15, 2025 na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini kuhusu Nini mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kiranjeranje-Nanjirinji-Ruangwa kwa kuanza kipande cha Kiranjeranje-Makanga?.

 

“Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Kiranjeranje-Makanga-Nanjirinji hadi Ruangwa yenye urefu wa kilometa 120 kwa kuanza na ujenzi wa madaraja makubwa matatu kwa kutumia fedha za dharura zilizotoka kwenye Mkopo nafuu wa Benki ya Dunia”, amesema Mhandisi Kasekenya.

 

Mhandisi Kasekenya ametaja madaraja hayo yakiwemo Daraja la Kigombo lenye urefu wa mita 25 na utekelezaji wake umefikia asilimia 25, Daraja la Nakiu lenye urefu wa mita 70 ambapo Mkandarasi yupo kwenye maandalizi ya ujenzi na  Daraja la Mbwemkuru 3 lenye urefu wa mita 100 ambalo lipo katika hatua ya mapitio ya usanifu.

 

Aidha, Mhandisi Kasekenya ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha ili iweze kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.