BARABARA YA SOMANGA MTAMA YAFUNGWA KWA MUDA, MTENDAJI MKUU TANROADS ATOA MAELEKEZO
Lindi
06 Machi, 2025
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi imetangaza kusitisha matumizi ya barabara ya Somanga Mtama kwa muda baada ya mvua kubwa zilizonyesha katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kuleta mafuriko makubwa yaliyoharibu eneo la barabara lilio kwenye njia ya mchepuko (diversion) ya ujenzi wa daraja la Somanga Mtama.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo, amesema kuwa maji yamejaa katika eneo hilo na kusababisha barabara kutoweza kupitika kwa sasa.
"Kwa sasa tumeshamjulisha Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, na ametoa maelekezo kuhusu usalama wa watumiaji wa barabara, jambo ambalo ni muhimu kabisa. Mtendaji Mkuu amelekeza barabara hii ifungwe ili kutoa nafasi ya kuchunguza hali ya uharibifu na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara. Tunawashauri wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zaidi kutoka mitandao ya kijamii ya TANROADS," alisema Mhandisi Zengo.
Mhandisi Zengo ameongeza kuwa vifaa vya kazi vipo kwenye eneo la tukio, na makandarasi wanaendelea na utekelezaji wa majukumu yao ili kurekebisha hali hiyo haraka.
"Maji yatakapopungua, tutaanza kufanya kazi ya kurejesha mawasiliano na barabara itafunguliwa mara moja," aliongeza.
Mhandisi Zengo amesisitiza kuwa usalama wa watumiaji wa barabara ni kipaumbele cha kwanza, na hivyo kuwalazimu kuifunga barabara hiyo kwa muda.
Aidha, amesema wananchi wataendelea kupewa taarifa rasmi kila hatua kuhusu maendeleo ya hali hiyo.