Bajaj, Pikipiki zaanza kupita daraja la Kinyerezi lililokatika
Dar es Salaam
29 Machi, 2025
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema njia ya muda (diversion) katika eneo la daraja la Kinyerezi sasa inaruhusu waenda kwa miguu, waendesha pikipiki na bajaji kupita, huku magari makubwa yakisubiri mpaka ujenzi ukamilike ndani ya siku mbili au tatu.Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Machi 29, 2025, jijini Dar es Salaam, Mhandisi Besta amesema mvua zinazoendelea ziliharibu sehemu ya tuta la muda, lakini TANROADS imechukua hatua za dharura kuhakikisha mawasiliano yanarejea haraka.“Kama mnavyojionea, wananchi wanapita kwa miguu na vyombo vyepesi vinapita, lakini kwa sasa magari makubwa yanapaswa kusubiri mpaka kazi ya kurejesha barabara ikamilike,” alisema na kuongeza"Tayari mkandarasi Kampuni ya Nyanza ameanza kazi ya kurejesha mawasiliano kwa kujaza udongo katika sehemu iliyoharibika, kuimarisha kingo za tuta, na kufunga kalvati za ziada ili kupunguza maji yanayopita eneo hilo. Timu ya wahandisi wa TANROADS iko eneo la kazi kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa haraka na kwa viwango vinavyotakiwa."Mhandisi Besta ameendelea kwa kusema kuwa, kwa sasa, wasafiri wanaoelekea Bonyokwa Center wanashauriwa kutumia barabara ya Kinyerezi inayopita Gereza la Segerea.Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeuhakikishia umma wa Watanzania kuwa, imejipanga kurejesha mawasiliano haraka katika maeneo yote yatakayokumbwa na maafa kutokana na mvua zinazoendelea.