News

MHA. KASEKENYA ATAKA MKAKATI WA KUKAMILISHA KAZI KWA WAKATI

MHA. KASEKENYA ATAKA MKAKATI WA KUKAMILISHA KAZI KWA WAKATI

 

Morogoro

27 Machi, 2025

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameutaka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kubuni mkakati utakaowezesha ujenzi wa barabara na madaraja nchini kukamilika kwa wakati.

 

Amesema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mkutano wa 20 wa baraza la wafanyakazi TANROADS na kusisitiza miradi ikikamilika kwa wakati itapunguza gharama za muda wa nyongeza na hivyo kuleta tija kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.

 

"Hakikisheni mnakuwa na  mkakati mahususi wa kusimamia wakandarasi ili wakamilishe ujenzi wa miradi kwa wakati na kutowapa mikataba mipya Makandarasi ambao hawajamaliza kazi zao kwa ufanisi", amesema Mha. Kasekenya.

 

Ameelezea umuhimu wa menejimenti kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwapa  mafunzo mbalimbali ili wawe wabunifu na wamudu kukabiliana na ukuaji wa mfumo wa teknolojia ya akili mnemba.

 

Mha.Kasekenya amemuzungumzia umuhimu wa  TANROADS kutoa elimu kwa watumishi na wananchi kuhusu utendaji kazi mizani za kupimia magari ili kujenga uelewa wa pamoja na kuondoa malalamiko katika jamii.

 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi la TANROADS Mha. Mohamed Besta amesema wamejipanga kuhakikisha wanasimamia miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja kwa ufanisi na kushirikiana na wakandarasi ili miradi ikamilike kwa wakati na ubora.

 

"Tutahakikisha tunasimamia vizuri mizani zetu ili zisiwe kikwazo katika kulinda barabara na madaraja na ukuaji wa sekta usafiri na uchukuzi nchini", amesema Mha. Besta.

 

Mha. Besta amesisitiza kuwa na ubunifu,  uhusiano na mawasiliano  mazuri kati ya memejimenti na watumishi yataendelezwa ili kuleta tija na ufanisi.

 

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bw. Musa Kilakala ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara ya Bigwa-Kisaki KM 78 na Barabara ya Ngerengere-Ubena Zomozi ambapo amesema zitafungua uchumi wa mkoa wa Morogoro na kuipongeza TANROADS kwa kufanya kazi kwa bidii.

 

Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi ambae ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw, Mrisho Mrisho amewataka watumishi wa TANROADS kuwa waadIlifu, kufanyakazi kwa kuzingatia miongozo ya Serikali,  kutoa huduma bora kwa umma bila upendeleo, kulinda  afya zao kwa kufanya mazoezi na kujikinga na maambukizi ya maradhi yanayoepukika.

 

Mkutano wa 20 wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS pamoja na mambo mengine unatarajiwa kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Wakala huo ya mwaka 2025/26.