KUFUATIA AGIZO LA WAZIRI ULEGA, KAMPUNI ZA UJENZI ZATII MAAGIZO, ZAAHIDI KUKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ameongoza kikao muhimu kati ya viongozi wa Serikali na viongozi wakuu wa kampuni za wakandarasi zinazotekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Nne (BRT4), madaraja pamoja na barabara nyingine nchini.
Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) leo Jumatano Machi 26, 2025, kufuatia ucheleweshaji wa miradi hiyo na malalamiko ya msongamano mkubwa wa magari katika maeneo husika.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Ulega amesema mkutano huo ni mwendelezo wa hatua alizochukua baada ya ziara yake ya Machi 4, 2025, ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya BRT4 na kupelekea wakandarasi waliokuwa eneo la mradi kukwama na kushindwa kutoa majibu ya msingi kuhusu ucheleweshaji wa kazi, jambo lililopelekea kuitwa kwa viongozi wakuu wa kampuni hizo kutoka makao makuu yao nchini China.
“Tuna furaha kuwa leo viongozi wa kampuni hizo wamefika Tanzania na tumepata nafasi ya kuzungumza nao. Wameeleza changamoto zao, ingawa hazilingani na muda mwingi uliopotezwa. Hata hivyo, tumeweka ahadi mpya za kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa,” alisema Waziri Ulega.
Katika kikao hicho, makampuni mbalimbali yalifanya ahadi za kimaandishi kwa Serikali kuhusu ukamilishaji wa miradi, Miongoni mwao ni kampuni ya Shandong, inayotekeleza ujenzi wa miundombinu ya BRT kutoka Mwenge hadi Tegeta.
Kampuni nyingine ni China Geo Corporation (CGC), inayojenga barabara ya kutoka Katikati ya Jiji hadi Mwenge na Mwenge hadi Ubungo kupitia barabara ya Sam Nujoma.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ameweka mkazo juu ya ucheleweshaji mkubwa wa kampuni ya Shandong kwenye mradi wa barabara ya Omurushaka - Kyerwa ambapo Viongozi wa kampuni hiyo wamekiri tatizo hilo na wameahidi kuanza kazi mwishoni mwa Aprili 2025, huku Waziri akipanga kufanya ukaguzi mwanzoni mwa Mei mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri Ulega, mradi wa BRT4 unapaswa kukamilika ifikapo Aprili 30, 2025, lakini wakandarasi wameomba nyongeza ya muda wa miezi 12.
Kufuatia hilo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inachakata ombi hilo kwa kuzingatia njia mbili: kuvunja mikataba au kuongeza muda kwa masharti madhubuti.
Kwa upande wao, wakandarasi wametaja changamoto kadhaa zilizosababisha ucheleweshaji, ikiwa ni pamoja na mvua za El Niño, ucheleweshaji wa kuhamishwa kwa nyaya za umeme, mabomba ya maji na gesi, ambazo si jukumu la mkandarasi.
Katika hilo, Waziri Ulega amesisitiza kuwa Taasisi za Serikali zinapaswa kushirikiana ili kuharakisha mchakato wa uhamishaji wa miundombinu hiyo.
Aidha, katika mradi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo hadi Kimara, Waziri amebainisha kuwa tatizo la matope wakati wa mvua litashughulikiwa mara moja na wataalamu wake.
Ili kupunguza msongamano wa magari katika maeneo yaliyoathirika na ucheleweshaji wa ujenzi wa BRT4, Waziri Ulega amesema wakandarasi wa kipande cha Mwenge hadi Tegeta wameahidi kuongeza sehemu za mgeuko (U-turns) na njia za mchepuko ndani ya wiki mbili zijazo.
Amebainisha kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano mkubwa kwenye barabara ya Mwenge – Tegeta, huku hatua zingine zikifanyika kwenye barabara ya Sam Nujoma hadi Ubungo, Ubungo hadi Mwenge na Mwenge hadi Morocco. Serikali pia itaendelea kufuatilia hatua hizi ili kuhakikisha zinapunguza usumbufu kwa wananchi.
“Kazi ya wataalamu wetu sasa ni kuhakikisha kwamba tunapata haki yetu kwa ucheleweshaji huu wa miradi. Ni suala la muda na miradi hii itakamilika kwa wakati ili wananchi waendelee kufurahia barabara zao,” alihitimisha Waziri Ulega huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwabana wakandarasi kuhakikisha kazi inafanyika kwa ufanisi.