News

UJENZI WA BARABARA YA KINTIKU - BAHI OVERPASS WAKAMILIKA, SASA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAGARI

UJENZI WA BARABARA YA KINTIKU - BAHI OVERPASS WAKAMILIKA, SASA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAGARI

 

Bahi

22 Machi, 2025

 

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa barabara ya lami katika eneo la Kitinku-Bahi umekamilika, hatua iliyopunguza msongamano wa magari katika eneo hilo.Akizungumza leo Jumamosi, Machi 22, 2025, Mhandisi Besta amesema barabara hiyo ni muhimu kwa magari yanayotoka na kwenda maeneo tofauti nchini, hivyo ukamilishaji wake utaimarisha usafiri na kupunguza changamoto zilizokuwepo.“Nimeridhishwa na kazi iliyofanywa na wataalamu wa TANROADS Mkoa wa Dodoma kwa kusimamia vizuri mkandarasi kuhakikisha changamoto ya msongamano inamalizika. Tunaomba radhi kwa usumbufu waliopata watumiaji wa barabara wakati wa ujenzi,” amesema Besta.Ameeleza kuwa alama za muda za barabarani tayari zimewekwa, na ndani ya wiki moja TANROADS itakamilisha uwekaji wa alama za kudumu ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo. Pia, amewataka madereva, hasa wa magari makubwa, kufuata sheria za barabarani na kuhakikisha wanazingatia alama za barabarani.Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Dodoma, Elisony Mweladzi, amesema foleni iliyokuwepo imeondolewa kabisa na akatoa wito kwa madereva kutunza barabara hiyo kwa kutoitupa taka ovyo, kumwaga mafuta, au kutengenezea magari barabarani.“Tunaomba madereva, hasa wa magari makubwa, waendeshe kwa kufuata alama za barabarani, hususan mwendo wa kilomita 50 kwa saa, wasitupe taka ovyo, na wasimwage mafuta barabarani,” amesema Mweladzi.Dereva wa lori, Hassan Hamis, amesema maboresho hayo yamewaondolea changamoto kubwa waliyoipata kwa muda mrefu.“Barabara hii ilikuwa na mabonde makubwa, hasa wakati wa mvua, lakini sasa hali ni nzuri. Tunashukuru sana Serikali kwa kutatua changamoto hii kwa haraka,” amesema.Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa eneo la Kitinku-Bahi, TANROADS kwa kushirikiana na TRC imeanza ujenzi wa barabara katika eneo la Mkonze, ambapo kazi ya kuimarisha miundombinu ya mapitio ya chini ya barabara na reli inaendelea.