News

UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA SHINYANGA WAFIKIA ASILIMIA 75, KUKAMILIKA JUNI 2025

UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA SHINYANGA WAFIKIA ASILIMIA 75, KUKAMILIKA JUNI 2025

 

Shinyanga

20/03/2025

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC), kuwa kiwanja cha ndege cha Shinyanga kitakamilika mwezi Juni mwaka 2025.

 

Amesema hadi sasa ujenzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 75 ambapo njia za kuruka na kutua ndege, maegesho na barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani hapo zimekamilika wakati jengo la abiria uko katika hatua nzuri za ujenzi..

 

"Mhe. Mwenyekiti kiwanja hiki kina urefu wa meta 2200 na upana wa meta 30 hivyo kitawezesha ndege aina ya Bombadier Q400 kutumia kiwanja hicho", amesema Dkt. Msonde.

 

Naibu Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 48.5 zitatumika katika ujenzi huo huku wananchi zaidi ya 240 wakipata ajira na kukamilika kwake kutachochea ukuaji wa shughuli za kilimo, madini na biashara.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge PIC, Augustine Vuma ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Wakala ya Barabara (TANROADS), kwa kazi nzuri na kuwahimiza kuhakikisha ujenzi unakamilika na huduma za usafiri wa ndege zinaanza mara moja.

 

" Kazi ni nzuri hakikisheni TANROADS, TAA na TCAA mnawasiliana vizuri ili huduma za usafiri wa anga mjini Shinyanga zianze mara moja", amesisitiza Mhe. Vuma.

 

Nae Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Julius Mtatiro amesema kukamilika kwa ujenzi wa kiwanja hicho kutaondoa adha kwa watumiaji wa huduma za ndege na kuchochea ukuaji wa Manispaa ya Shinyanga.