News

PIC YARIDHISHWA KASI UJENZI WA BARABARA KIGOMA

PIC YARIDHISHWA KASI UJENZI WA BARABARA KIGOMA Kigoma 18 Machi, 2025 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imeridhishwa na ujenzi wa barabara ya Kasulu - Kabingo yenye urefu wa Kilometa 260, inayotekelezwa kwa awamu nne kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 400 mkoani Kigoma. Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Augustine Vuma, amesema kamati imekagua na kuridhika na maendeleo ya ujenzi huo, ambao umefikia asilimia 83. Ameeleza kuwa ujenzi wa sehemu zote nne kwa wakati mmoja katika mkoa mmoja ni jambo la kipekee, na ameitaka Wizara ya Ujenzi na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati. Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameeleza kuwa, miradi hiyo inagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ambapo mikataba ilisainiwa kati ya mwaka 2020 na 2022, na muda wa utekelezaji umepangwa kuwa miezi 36 kwa kila awamu. Kwa mujibu wa taarifa ya TANROADS, utekelezaji wa ujenzi wa barabara hizo umeendelea kwa viwango tofauti. Barabara ya Kasulu - Manyovu yenye urefu wa kilomita 68.25 imefikia asilimia 84.63 na inatarajiwa kukamilika Mei 30, 2025. Ujenzi wa barabara ya Kanyani Junction - Mvugwe yenye urefu wa kilomita 70.5 umefikia asilimia 75.38 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 30, 2025. Aidha, ujenzi wa barabara ya Mvugwe - Nduta Junction yenye urefu wa kilomita 59.35 umefikia asilimia 90.75 na utakamilika Mei 7, 2025. Kwa upande wa barabara ya Nduta Junction - Kabingo yenye urefu wa kilomita 62.50, ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100. Miradi hii ya barabara inatarajiwa kuimarisha uchumi wa mkoa wa Kigoma kwa kuboresha usafiri wa ndani na wa nje, kwani barabara hizo ni sehemu ya mtandao wa ushoroba wa Magharibi unaounganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.