News

KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA KASI UJENZI DARAJA LA PANGANI

KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA KASI UJENZI DARAJA LA PANGANI

 

Pangani

14 Machi, 2025

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja la Pangani.

 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Seleman Moshi Kakoso amesema kazi iliyofanywa kwenye daraja hilo lenye urefu wa meta 525 ni kubwa hivyo Wizara ya Ujenzi na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), wahakikishe daraja hilo linakamilika kwa wakati, ili kukuza fursa za uwekezaji katika ushoroba wa fukwe za mikoa ya Tanga na Pwani.

 

“Hakikisheni kasi ya ujenzi wa daraja iendane na ujenzi wa barabara ili vikamilike na kutoa huduma mara moja", amesema Kakoso.

 

Kamati hiyo inayoendelea na ukaguzi wa miradi ya kimkakati katika mkoa wa Tanga  imekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani- Bagamoyo Km 256 ambayo ujenzi wake unaendelea.

 

Naibu Waziri wa  Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameihakikishia Kamati hiyo ya Bunge kuwa barabara ya Tanga-Pangani ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 75 itakamilika Juni mwaka huu.

 

" Tumejipanga kuhakikisha sehemu hii ya kwanza Tanga-Pangani inakamilika ifikapo mwezi Juni wakati daraja likitarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu", amebainisha Naibu Waziri mha. Kasekenya.

 

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mha. Mohamed Besta amesema ujenzi huo umegawanywa katika sehemu nne ili kuharakisha ujenzi wake.

 

Amezitaja sehemu hizo kuwa ni Tanga-Pangani km 50, daraja la Pangani meta 525 na barabara unganishi km 25.6, barabara ya Mkange-Mkwaja-Tungamaa km 95.2 na sehemu ya Mkange-Bagamoyo Makurunge km 73.25 ambayo usanifu wake umekamilika.

 

Kukamilika kwa barabara hii  kutachochea ukuaji wa uchumi, kupunguza gharama na muda wa safari, kuwezesha kufikika kwa urahisi vivutio vya utalii na kuunganisha kwa njia fupi bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa.