News

UJENZI WA BARABARA YA KIMARA - MAVURUNZA - BONYOKWA - KINYEREZI KWA KIWANGO CHA LAMI WAANZA

UJENZI WA BARABARA YA KIMARA - MAVURUNZA - BONYOKWA - KINYEREZI KWA KIWANGO CHA LAMI WAANZA Dar es Salaam 11 Machi, 2025 Baada ya kukamilika kwa maandalizi muhimu, ujenzi wa Barabara ya Kimara - Mavurunza - Bonyokwa hadi Kinyerezi kwa kiwango cha lami umeanza rasmi. Kazi za ujenzi zinaendelea kwa kasi, hatua inayotarajiwa kuleta maboresho makubwa katika sekta ya usafiri na uchumi wa eneo hilo. Barabara hii yenye urefu wa kilometa 7 ni barabara ya kimkakati, inayotarajiwa kuwa kiunganishi muhimu kati ya majimbo ya Ubungo na Segerea. Mradi huu unatekelezwa na kampuni ya kizawa ya Nyanza Road Works, ambayo imeshika dhamana ya ujenzi wa barabara hiyo muhimu na ya kimkakati. Wakiongea kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo ya Kimara, Bonyokwa, Kinyerezi, na maeneo jirani wameeleza kuwa, wana matumaini makubwa kuwa ujenzi huu utapunguza changamoto za miundombinu na usafiri. Pia, wanatarajia kunufaika kiuchumi kupitia fursa zitakazotokana na mradi huu, ikiwemo biashara na huduma nyingine zinazotokana na uboreshwaji miundombinu bora ya barabara. Ujenzi huo unajumuisha daraja kubwa lenye urefu wa mita 25, pamoja na madaraja madogo saba ya kalvati, ambayo yatasaidia kupitisha maji wakati wa mvua kubwa. Pia, mkandarasi anahitajika kufunga taa za barabarani, hatua inayolenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara hii. Huu ni mradi wa kihistoria unaolenga kuimarisha miundombinu ya jiji, kuboresha huduma za usafiri, na kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa maeneo husika.