SERIKALI YABORESHA MIUNDOMBINU KUUNGANISHA TANZANIA NA KENYA-MHA. BESTA
26th February, 2025
SERIKALI YABORESHA MIUNDOMBINU KUUNGANISHA TANZANIA NA KENYA-MHA. BESTA
Tanga
26 Feb, 2025
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu muhimu kwa ajili ya kuimarisha usafirishaji na uchumi wa wananchi, hususan katika ukanda wa Pwani ya Mashariki.
Hayo yamejidhihirisha kupitia mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Mkange) - Pangani - Tanga yenye urefu wa kilometa 256, ikijumuisha Daraja la Mto Pangani lenye urefu wa mita 525, ambao unalenga kuunganisha Tanzania na Kenya kupitia mtandao wa barabara za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta akitoa taarifa fupi ya mradi huo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yupo kwenye ziara mkoani Tanga, amesema, mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) pamoja na Serikali ya Tanzania na umepewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake wa kiuchumi.
Mradi huu unatekelezwa katika sehemu nne kuu, ambapo maendeleo yake yanaendelea kwa kasi.
Sehemu ya kwanza ni barabara ya Tanga - Pangani yenye urefu wa kilometa 50, ambayo inatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 118.7 na imefikia asilimia 75 ya utekelezaji. Barabara hii itarahisisha usafiri na biashara kati ya mikoa ya Pwani na Tanga.
Sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa Daraja la Mto Pangani lenye urefu wa mita 525 pamoja na barabara za maungio, mradi unaogharimu shilingi bilioni 107, huku ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 53. Daraja hili litaimarisha mawasiliano na uchumi wa maeneo yanayozunguka Mto Pangani.
Sehemu ya tatu ni ujenzi wa barabara ya Mkange - Mkaja - Tungamaa yenye urefu wa kilometa 95 pamoja na barabara za Kipumbwi. Ujenzi wa sehemu hii unagharimu shilingi bilioni 123 na umefikia asilimia 46 ya utekelezaji. Barabara hii itaboresha usafiri na kuunganisha jamii za vijijini na masoko makubwa.
Kwa upande wa sehemu ya nne, mazungumzo kati ya Serikali na AfDB yanaendelea ili kupata ufadhili wa ujenzi wa barabara ya Makurunge - Mkange yenye urefu wa kilometa 73. Hatua hii ni muhimu katika kukamilisha mtandao wa barabara unaounganisha ukanda wa Pwani ya Mashariki.