News

TRILION 2.7 ZALETA MAGEUZI MAKUBWA YA MIUNDOMBINU YA BARABARA TANZANIA

TRILION 2.7 ZALETA MAGEUZI MAKUBWA YA MIUNDOMBINU YA BARABARA TANZANIA Tanga 26 Feb, 2025 Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ameelezea mafanikio makubwa ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa miundombinu, akisema kuwa kilometa 1,366 za barabara zenye thamani ya shilingi trilioni 2.7 zimekamilika nchini, huku madaraja makubwa yakijengwa na kukamilika kwa kasi ya hali ya juu. Akizungumza leo Februari 26, 2025, katika mkutano wa hadhara wilayani Pangani mkoani Tanga, ambapo mgeni rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Ulega amesema kuwa serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha maendeleo yanafika kwa wananchi wote. "Ulipoingia madarakani, ulikuta barabara na madaraja yakiendelea kujengwa. Kwa kauli yako ya Kazi Iendelee, madaraja manane yenye thamani ya shilingi bilioni 381 umeyakamilisha, yakiwemo Tanzanite, Kitengule, na Msingi pale Singida. Haya yote ni mapinduzi makubwa kwa Watanzania,” alisema Ulega. Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameeleza kuwa miradi mikubwa ya barabara inaendelea kwa kasi, ikiwemo ujenzi wa kilometa 2,031 za barabara zenye thamani kubwa kwa taifa. "Barabara ya Bagamoyo (Makurunge) - Mkange - Tungamaa - Pangani - Tanga inayoendelea kujengwa ni ushahidi wa dhamira yako thabiti Mheshimiwa Rais. Barabara hii itaunganisha mikoa na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Bagamoyo, Chalinze, Pangani na Tanga,” alieleza. Waziri Ulega pia amezungumzia ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525, ambalo litakuwa na taa 240 za barabarani, huku mji wa Pangani ukipata taa 200 zaidi, kuhakikisha usalama wa wananchi na kuboresha mandhari ya eneo hilo. "Kama haitoshi, umeweka msisitizo kwamba kila barabara inayojengwa iwe na taa za barabarani. Wizara ya Ujenzi imechukua agizo lako kwa uzito mkubwa, na tunahakikisha kila mradi unakamilika kwa viwango vya juu,” alisema. Akitilia mkazo kasi ya ujenzi wa miradi hiyo, Waziri Ulega amesema kuwa wakandarasi wanahimizwa kufanya kazi bila kusita. "Wakandarasi hawatudai sisi, bali sisi tunawadai kazi. Hapa hakuna kucheka, hakuna relax mpaka kazi ikamilike. Tutasimamia kila kitu usiku na mchana kwa maendeleo ya Watanzania," alisisitiza Ulega.