News

AfDB YADHAMIRIA KUUNGANISHA AFRIKA KWA MIUNDOMBINU YA KIMKAKATI

AfDB YADHAMIRIA KUUNGANISHA AFRIKA KWA MIUNDOMBINU YA KIMKAKATI Tanga 26 Feb, 2025 Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley, amesema benki hiyo imejipanga kuendelea kufadhili miradi mikubwa ya miundombinu ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuunganisha Afrika kwa barabara, madaraja, viwanja vya ndege na njia za usafirishaji wa bidhaa. Akizungumza Jumatano, Februari 26, 2025, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge) - Pangani - Tanga, sehemu ya Mkange - Pangani - Tanga yenye urefu wa kilometa 170.8 pamoja na Daraja la Mto Pangani, Dkt. Laverley amesema mradi huo unatoa msukumo mkubwa kwa ushirikiano wa Tanzania na Kenya. "Kwa niaba ya Benki ya Maendeleo ya Afrika, nimepokea kwa furaha fursa hii ya kushuhudia hafla hii ambayo inatoa msukumo kwa nchi za Kenya na Tanzania wa kujenga barabara ya kutoka Bagamoyo hadi Tanga hadi Horohoro kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya," alisema. Ameeleza kuwa jiwe la msingi lililowekwa katika mradi huo ni kielelezo cha ndoto ya kihistoria ya kuunganisha miji ya Lamu, Malindi na Mombasa kwa upande wa Kenya na Tanga, Dar es Salaam, na Mtwara kwa upande wa Tanzania. Dkt. Laverley amesisitiza kuwa Tanzania, ikiwa na eneo la kilometa za mraba 950,000, inapaswa kuendelea na juhudi za kujenga madaraja ya kisasa na viwanja vya ndege vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege wa Tanga, ambao AfDB inafurahia kuwa sehemu ya utekelezaji wake. Aliongeza kuwa miradi inayofadhiliwa na benki hiyo inalenga kuunganisha njia kuu za uchumi wa bara la Afrika, huku akisisitiza dhamira ya AfDB ya kuunganisha Afrika kutoka Jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Jiji la Cairo nchini Misri.