MAKONDA: HAKUNA BARABARA MPYA KUJENGWA BILA KUWA NA MPANGO WA UPANDAJI MITI
Arusha
15 Februari, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameelekeza kwa taasisi za Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha kuwa kila barabara mpya inayojengwa inakuwa na mpango mkakati wa kupanda miti.
Alitoa agizo hilo tarehe 15 Februari, mwaka huu alipoongoza wananchi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo katika kampeni maalum ya usafi wa mazingira na upandaji miti kata ya Ambureni, Halmashauri ya Meru ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuzaliwa kwake.
Makonda amesema kuwa, haitakubalika kukata miti kwa ajili ya ujenzi wa barabara bila kuhakikisha miti mingine inapandwa ili kulinda mazingira.
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa mchakato wa ukaguzi wa barabara mpya utahusisha pia tathmini ya upandaji miti, sawa na jinsi taa za barabarani zinavyokaguliwa.
"Kama tunavyoweka taa barabarani, lazima pia kuwe na eneo la upandaji miti. Hii ni kuhakikisha mji wetu wa Arusha unaendelea kutunza mazingira kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan," alisema Makonda.
Hatua hii inalenga kuimarisha mazingira ya Arusha, mji unaojulikana kwa mandhari yake ya asili, kitovu cha utalii huku ukiendelea kukua kwa kasi kiuchumi.