WAZIRI APONGEZA KASI YA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA, AAGIZA KUFUNGWA TAA ZA KUONGOZEA NDEGE HARAKA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amepongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga na kuagiza mkandarasi CHICO kuhakikisha taa za kuongozea ndege zinafungwa mara moja.
Mheshimiwa Majaliwa alitoa agizo hilo Februari 16, 2025 alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo na kuelekeza kuwa uwanja huo tayari umekamilika, isipokuwa taa za kuongozea ndege, na hivyo jengo la zamani la abiria litumike kwa sasa wakati jengo jipya linaendelea kukamilika.
Aidha, Waziri Mkuu alipongeza kazi nzuri inayofanywa na mkandarasi CHICO chini ya usimamizi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na kusisitiza kuwa mkandarasi aendelee kusimamiwa ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Samuel Joel Mwambungu, alieleza kuwa, utekelezaji wa mradi huo unaendelea vizuri, ambapo njia ya kurukia na kutua ndege (Runway), njia ya kuingia na kutokea ndege (Taxiway), pamoja na sehemu ya maegesho ya ndege (Apron) zimekamilika kwa asilimia 100 huku ujenzi wa jengo la abiria (Terminal Building) ukifikia asilimia 50 na unaendelea vyema.
Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyannga wenye urefu wa Kilometa 2.2 unafadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo ni moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mkoa huo na mikoa jirani.