News

TANROADS, ITALIA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA

TANROADS, ITALIA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA

 

Dar es Salaam

11 Februari, 2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imesema itashirikiana na nchi ya  Italia katika kuendeleza sekta ya Miundombinu ya Barabara na madaraja makubwa nchini.

 

Hayo yamesemwa leo tarehe 11 Februari, 2025 na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta katika Kongamano la Nne la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia linalofanyika kwa siku mbili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

 

Mha. Besta amesema taasisi yake inayosimamia miundombinu imenufaika na kongamano hilo, ambapo wamejenga mashirikiano na Italia katika kufanya kazi Pamoja za ujenzi wa miundombinu.

 

“Tunaishukuru serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje waliotualika kushiriki kwenye kongamano hili na tumekuwa na mazungumzo mazuri na wenzetu wa Italia, pia mashirika mbalimbali yanayotoa fedha na yanayohusika na ujenzi wa miundombinu kwenye nchi hiyo, na kwa kifupi tumekubaliana kuendeleza mashirikiano hayo kwa vitendo, kwa wao kuona ni maeneo gani wanaweza kushiriki kwa kutoa fedha, teknolojia na kuwajengea uwezo wataalam wa TANROADS,” amesisitiza Mha. Besta.

 

Amesema mbali na kuendeleza mashirikiano hayo, pia amewaeleza namna serikali ya Tanzania inavyodhamiria kushirikiana na Sekta binafsi na mashirika yenye kutoa fedha zenye unafuu katika ujenzi wa miundombinu ya Barabara (Public and Private Parterships-PPP), ambapo TANROADS inamiradi kadhaa itakayofanywa kwa mfumo huo.

MWISHO