News

ZINGATIENI UBORA BARABARA YA KAHAMA- KAKOLA KM 73

ZINGATIENI UBORA BARABARA YA KAHAMA- KAKOLA KM 73

Kahama

10 Feb, 2025

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameelekeza kwa Mkandarasi China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC), anayejenga barabara ya Kahama-Kakola Km 73 kujenga kwa kuzingatia viwango vya ubora ili kuiwezesha barabara hiyo kudumu kwa muda mrefu.

 

Akikagua ujenzi huo leo Mha. Kasekenya amesema barabara hiyo inayopita katika eneo lenye mbuga na maji mengi inatakiwa ijengwe kukidhi usanifu wake na hivyo kukuza uchumi wa wakazi wa mikoa ya Shinyanga na Geita.

 

"TECU hakikisheni barabara hii inakuwa kielelezo cha kazi nzuri mlizofanya ili ziwanadi ndani na nje ya nchi", amesisitiza Naibu Waziri huyo.

 

Amesema nia ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuiunganisha barabara yote kwa lami kutoka Kahama-Kakola-Ilogi hadi Geita Km 118 na hivyo kuinganisha kwa njia fupi mikoa ya Shinyanga na Geita na kuongeza barabara za kisasa katika Ukanda wa Ziwa.

 

Kasekenya amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Bi. Mboni Mhita kuhakikisha usalama kwa mkandarasi na mali zake unaimarishwa na kutoa elimu kwa wananchi  ili kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara.

 

"Hakikisheni shughuli za kilimo, uchungaji na ujenzi kwenye hifadhi ya barabara unadhibitiwa ili ujenzi uende kama ulivyopangwa", amesisitiza Naibu Waziri Kasekenya.

 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Bi. Mboni Mhita amesema barabara hiyo itakapokamilika itachochea ukuaji wa miji ya Kahama na Geita na kuongeza uzalishaji wa mpunga na uchimbaji wa madini na hivyo kukuza uchumi wa wakazi wa mikoa hiyo.

 

Kwa upande wake Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga Mha. Joel Mwambungu amesema zaidi ya shilingi bilioni 100.6 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo, watu 408 waliopisha ujenzi watalipwa fidia mapema na zaidi ya watanzania 299 wamepata ajira hadi sasa.

 

"Tumejipanga kuweka taa kwenye maeneo yote yenye miji katika barabara hii ili kuchochea huduma na biashara kufanyika usiku na mchana", amesema Mha. Mwambungu.

 

Naibu Waziri Kasekenya amehitimisha ziara yake ya siku mbili kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu katika mikoa ya Tabora na Shinyanga.