News

KIWANJA CHA NDEGE TABORA KUKAMILIKA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI

KIWANJA CHA NDEGE TABORA KUKAMILIKA MWISHO WA MWEZI FEBRUARI

 

Tabora

09 Feb, 2025

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amemueleza mkandarasi M/s Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd (BCEG), anaejenga Kiwanja cha ndege cha Tabora kuhakikisha wanaongeza bidii ya ujenzi ili uweze kukamilika Februari 28 mwaka huu.

 

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo Mha. Kasekenya ameelezea kuridhishwa na hatua iliyofikiwa ya asilimia 90 hadi sasa.

 

"Mkifanya bidii asilimia 10 zilizobaki mtakamilisha ndani ya mwezi huu na hivyo kutupa fursa ya kuwaalika viongozi wakuu kuja kufungua kiwanja hiki”, amesema Mha. Kasekenya.

 

Naibu Waziri huyo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Shillingi Bilioni 24.6 kukarabati na kuboresha kiwanja hicho na kusisitiza umuhimu wa wananchi wa mkoa wa Tabora kuibua fursa za uwekezaji na biashara zitakazosababishwa na uwepo wa kiwanja cha ndege cha kisasa.

 

Amesema katika kurahisisha usafiri wa anga katika mikoa ya Kanda ya Magharibi viwanja vya ndege vya Kigoma, Sumbawanga na Shinyanga navyo vinajegwa sambamba na Tabora.

 

Amemuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Tabora Mha. Rafael Mlimaji kuhakikisha kukamilika kwa kiwanja hicho kunaendana na barabara bora za kwenda katika kiwanja hicho ili kuleta tija.

 

Mha. Mlimaji amesema kukamilika kwa ujenzi huo unaohusisha jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege, maegesho,, uzio, kituo cha hali ya hewa na barabara za kuingia kiwanjani utachochea uchumi wa mkoa wa Tabora.

 

"Kiwanja hiki kitarahisisha huduma za usafiri, kukuza biashara, kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kukuza utalii", amesisitiza Mha. Mlimaji.