News

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA MWENENDO WA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA MSALATO

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YARIDHISHWA NA MWENENDO WA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA MSALATO

Dodoma

08 Februari, 2025

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unaendelea kwa kasi, huku sehemu ya njia ya kuruka na kutua ndege (runway) ikiwa imefikia asilimia 90 ya utekelezaji.

 

Hii ni hatua muhimu kuelekea kukamilika kwa mradi huu mkubwa wa miundombinu unaotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo, ikisema kuwa serikali inapaswa kuhakikisha mkandarasi anamaliza kazi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, amepongeza juhudi za serikali katika kufanikisha mradi huu na kusisitiza kuwa ucheleweshaji wa kazi haukubaliki, kwani huongeza gharama zisizo za lazima.

 

Kamati hiyo pia imeitaka serikali kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwanja wa ndege yanalindwa dhidi ya uvamizi wa wananchi, kwani mara nyingi watu huanza kujenga kiholela na kufanya uwekezaji usio rasmi, hali inayosababisha changamoto kubwa katika kuwaondoa na gharama za fidia kwa serikali.

 

“Tunasisitiza maeneo haya yahifadhiwe mapema ili kuepuka matatizo ya baadaye. Tukiruhusu uvamizi, serikali italazimika kuwalipa fidia wakazi waliovamia, jambo ambalo linaweza kuchelewesha mradi,” alisema Kakoso.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa Wizara ya Ujenzi, kwa kushirikiana na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), inahakikisha kuwa ujenzi wa uwanja huu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa.

 

 

Mhandisi Kasekenya amesisitiza kuwa serikali itamsimamia mkandarasi kikamilifu kuhakikisha uwanja unajengwa kwa mujibu wa mkataba.

 

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, sehemu ya njia ya kuruka na kutua ndege (runway) imefikia asilimia 90 ya utekelezaji.

 

 Hii inamaanisha kuwa iwapo kutakuwa na dharura yoyote, runway hiyo inaweza kutumika. Hata hivyo, kazi inaendelea kuhakikisha sehemu zote za uwanja zinakamilika kwa wakati.

 

Mbali na runway, ujenzi wa njia za kuingilia na kutoka kwa ndege (taxiways) pia unaendelea kwa kasi, huku tabaka la mwisho la lami likiendelea kuwekwa.

 

“Kwa sasa tumeshajenga taxiways mbili, lakini tutaongeza zaidi kadri mahitaji yatakavyoongezeka,” alisema Besta.

 

Serikali imeeleza mpango wake wa kuhakikisha uwanja huu wa kimataifa unaunganishwa na njia bora za usafiri wa reli na barabara.

 

Kamati ya Bunge imesisitiza kuwa ni muhimu uwanja huu uunganishwe na Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na barabara za kisasa za mchepuko ili kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dodoma.

 

"Uwanja huu utakapokamilika, ni lazima kuwe na miundombinu inayorahisisha usafiri wa abiria na mizigo kutoka na kuingia Dodoma kwa urahisi. Hii ni fursa ya kulifanya jiji hili kuwa kitovu cha biashara na uchumi," alieleza Kakoso.

 

Mbali na kuhudumia abiria wa ndani na nje ya nchi, uwanja huu utakuwa na miundombinu maalum kwa ajili ya kusafirisha mazao ya kilimo, mbogamboga na matunda kwenda masoko ya kimataifa.

 

Kamati ya Bunge imependekeza uwekezaji katika maeneo maalum ya kuhifadhi bidhaa zinazoharibika haraka (cold rooms) ili kusaidia wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza mazao yao nje ya nchi kwa urahisi zaidi.

 

"Kwa mara ya kwanza, Tanzania itakuwa na uwanja wa ndege wenye miundombinu ya kisasa kwa ajili ya kusafirisha bidhaa moja kwa moja kwenda masoko ya nje. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara wetu," alisema Kakoso.

 

Serikali imehakikisha kuwa uwanja huu utakuwa na jengo la kuongozea ndege (control tower) refu zaidi kwa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ni la sita kwa ukubwa barani Afrika.

 

 Pia, vifaa vyake vitakuwa vya kisasa zaidi kuliko viwanja vyote vya Tanzania, jambo linaloifanya Dodoma kuwa kitovu kipya cha safari za kimataifa.

 

Kwa mujibu wa serikali, hatua za mwisho za kukamilisha uwanja huu zinatarajiwa kufanyika kati ya Julai na Agosti mwaka huu, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kukamilika kwake rasmi.

 

Serikali imewataka Watanzania na wawekezaji mbalimbali kuanza kujiandaa kutumia fursa za kiuchumi zitakazotokana na uwanja huu wa kimataifa, kwani utafungua milango ya biashara, utalii, na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi kwa urahisi mkubwa.

 

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato si tu utarahisisha safari za ndani na nje ya nchi, bali pia utaifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha usafiri wa anga, biashara na uwekezaji nchini Tanzania.