News

TANROADS MKOA WA MTWARA WAREJESHA MAWASILIANO KATIKA BARABARA YA DAR - MTWARA

TANROADS MKOA WA MTWARA WAREJESHA MAWASILIANO KATIKA BARABARA YA DAR - MTWARA

 

Mtwara

07 Feb, 2025

Usafiri kati ya Mtwara na Dar es Salaam uliokuwa umesimama kutokana na tope zito kujaa barabarani eneo la Mikindani, umerejea katika hali ya kawaida baada ya barabara kuu kufunguka.

 

Jitihada za makusudi zimefanywa na ofisi ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na wananchi kusafisha tope lililosababisha magari kukwama kwa kushindwa kupita kwenye eneo hilo. Safari zimerejea leo tarehe 7 Februari, 2025 majira ya saa 2:00 asubuhi. 

 

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Mtwara zilisababisha maporomoko ya tope yaliyofunika barabara, na kusababisha usumbufu kwa wasafiri na wasafirishaji.

 

Hali hiyo ilianza alfajiri ya leo, Februari 7, 2025, lakini hatua za haraka zilizochukuliwa na TANROADS Mtwara zimefanikisha urejeshaji wa usafiri. 

 

Licha ya barabara kuwa wazi kwa sasa, tahadhari inatolewa kwa madereva na wasafiri kuwa makini kwa kuwa barabara hiyo imekuwa na utelezi unaosababishwa na mvua zinazoendelea.