News

TANROADS MANYARA YAFANYA MAREKEBISHO YA MABEGA YA BARABARA YA BABATI-MINJINGU

TANROADS MANYARA YAFANYA MAREKEBISHO YA MABEGA YA BARABARA YA BABATI-MINJINGU

 

Manyara

25 Januari, 2025

Ofisi ya Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara inaendelea na kazi ya matengenezo ya mabega ya barabara ya Babati–Minjingu, barabara kuu inayounganisha mikoa ya Arusha na Manyara. Matengenezo hayo, yanayojumuisha marekebisho ya mabega ya barabara (shoulder repair), yanafanyika ili kuhifadhi uimara wa barabara hiyo ambayo imeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha. Mabega ya barabara hiyo yameharibiwa kwa kiasi kikubwa na maji , hivyo hatua za haraka zimechukuliwa ili kuzuia uharibifu zaidi na kuhakikisha barabara inapitika muda wote. Kazi ya ukarabati inatekelezwa katika Kijiji cha Kiongozi, kilichopo wilayani Babati. Shughuli hizo zinahusisha ujenzi wa mabega kwa kutumia zege, ambayo itasaidia kuimarisha kingo za barabara na kuzuia maji kuendelea kuharibu miundombinu. Barabara ya Babati–Minjingu ni kiungo muhimu kinachochangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Manyara kwa kuunganisha mkoa huo na Dodoma ambayo ni makao makuu ya nchi.