News

UJENZI WA MAEGESHO YA MAGARI NA TAA ZA BARABARANI WANUKIA DAKAWA NA KIBAIGWA

UJENZI WA MAEGESHO YA MAGARI NA TAA ZA BARABARANI WANUKIA DAKAWA NA KIBAIGWA

Kibaigwa

13 Januari, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza kujengwa kwa maegesho ya malori na taa za barabarani katika miji ya Dakawa na Kibaigwa katika barabara ya Morogoro – Dodoma, ili kupunguza ajali na kukuza biashara katika miji hiyo.

 

Akikagua barabara hiyo Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewaelekeza Mameneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS ) wa mkoa ya Morogoro na Dodoma kutekeleza agizo hilo..

 

"Mhe. Rais amenielekeza tuhakikishe kwenye barabara kuu nchini kote tunafunga taa za barabarani zinazotumia umeme wa jua (solar) katika miji inayokuwa ili kuongeza usalama, kupunguza ajali na kuimarisha biashara za wananchi wa maeneo hayo", amesisitiza Waziri Ulega.

 

Waziri Ulega amesema Mameneja wote wahakikishe miji inang’aa kwa taa za umeme jua (Solar), ambazo ni gharama nafuu na kusisitiza kuwa barabara nzuri ni fursa hivyo zikiboreshwa zitachochea maendeleo na kukuza biashara haraka.

 

"Katika kupunguza msongamano wa magari Morogoro mjini tutajenga barabara wezeshi kati ya eneo la Nanenane - Msamvu na Kihonda - Mkundi tunaomba wananchi mtupe ushirikiano ili eneo hilo liboreshwe", amesisitiza Ulega.

 

Amesema barabara ya Stesheni hadi Kihonda inajengwa kwa njia nne ili kupunguza msongamano na kuvutia uwekezaji.

 

Amemtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba kuanza ujenzi wa maegesho lenye urefu wa mita 200 na kufunga taa 50 za umeme wa jua eneo la Dakawa na Mha. Zuhura Aman wa mkoa wa Dodoma kufanya hivyo eneo la Kibaigwa ili kupendezesha miji hiyo na kuchochea biashara ili zifanyike pia nyakati za usiku.

 

Aidha, Ulega amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, kuhakikisha ujenzi wa miradi ya dharura unaambatana na uwekaji wa taa za barabarani ili kuimarisha usalama na kupendezesha jiji na kujenga barabara za mchepuko ili kuondoa msongamano wa magari katikati ya jiji la Dodoma.

 

Kuhusu ujenzi wa miradi ya dharura Waziri Ulega amesema Serikali imetoa Bilioni 54 kwa ajili ya kukarabati madaraja yalioathirika na mvua za el-nino mkoani Morogoro na zaidi ya Bilioni 35 mkoani Dodoma hivyo kuwataka wakandarasi waliopewa miradi hiyo kuongeza kasi ya ujenzi na kufanya kazi usiku na mchana.