News

MKANDARASI WA UJENZI BARABARA YA LUSAHUNGA – RUSUMO ATAKIWA KUONGEZA KASI

MKANDARASI WA UJENZI BARABARA YA LUSAHUNGA – RUSUMO ATAKIWA KUONGEZA KASI

Rusumo

13 Januari, 2025

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka Mkandarasi M/S China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya Lusahunga-Rusumo (Km 92) kwa kiwango cha lami.

 

Mhandisi Kasekenya ametoa agizo hilo tarehe 13 Januari 2025, Mkoani Kagera wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo ameridhishwa na hatua za ujenzi wa mradi huo.

 

“Kazi inaonekana imeanza vizuri, hivyo Mhandisi Msimamizi uhakikishe unamsimamia Mkandarasi kwa ukaribu kwa kuongeza mitambo, wafanyakazi  na kuongeza masaa ya kazi ili kazi iweze kukamilika kwa muda uliopangwa”, amesema Mhandisi Kasekenya.

 

Ameongeza kuwa Mkandarasi CCECC ni kampuni kubwa inayoaminiwa na Serikali kwenye suala zima la ufanisi wa kazi kwani wanafanyakazi nzuri na kazi kubwa wakisimamiwa vizuri.

 

Aidha, amesema barabara ya Lusahunga-Rusumo ni kati ya barabara kubwa ambayo inategemewa katika uchumi wa Taifa kwani inaunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kongo.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya amesema maendeleo ya ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 20, na ameahidi kumsimamia Mkandarasi huyo ili aweze kukamilisha kazi kwa wakati uliopangwa.

 

Vilevile amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutasaidia kuboresha huduma za usafirishaji wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji kwa magari ya usafirishaji bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi jirani.