MIRADI YA DHARURA IJENGWE KWA KASI NA UBORA - WAZIRI ULEGA.
Lindi
10 Jan, 2025
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameelekeza miradi ya dharura inayojengwa sasa ijengwe kwa kasi, iwe ya viwango, na kuzingatia thamani ya fedha.
Ametoa kauli hiyo katika Kata ya Tingi Wilayani Kilwa mkoani Lindi alipokagua maendeleo ya ujenzi katika maeneo yalioathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya vilivyuotokea mwaka 2024.
" Zaidi ya Shilingi Bilioni 114, zimeletwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi 13 ya barabara na madaraja mkoani Lindi, hivyo TANROADS zisimamieni fedha hizo ili zilete tija", amesema Ulega.
Waziri Ulega amefurahishwa na kasi ya ujenzi ya mkandarasi China Henan anayejenga sehemu ya Somanga na Mkandarasi mzawa Makapo anayejenga daraja la Mikereng'ende ambaye amefikia asilimia 25 ya ujenzi wa daraja hilo na kusisitiza nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuendeleza wakandarasi wazawa.
"Kila mkandarasi awe na mikakati ya ujenzi itakayomwezesha kuendelea na ujenzi wakati wa mvua za masika ili miradi isisimame", amesema Ulega,.
Hakikisheni vifaa,mitambo na wafanyakazi wanakuwepo ili kazi zifanywe usiku na mchana na kipaumbele kwa kazi zisizo za ujuzi wapewe wananchi wenyeji.
Aidha, Waziri Ulega ameelekeza kwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha kunawekwa taa za barabarani katika eneo la Somanga na Njia Nne ili kuwawezesha wananchi kufanya biashara usiku pia.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mohammed Nyundo amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya dharura.
Naye Diwani wa Kata ya Tingi Rajab Ngatanda amemuomba Waziri Ulega ujenzi wa Barabara ya Njia nne - Matapata kwa kiwango cha Changarawe ili iweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka.