News

TANROADS YAANZA KUREJESHA MAWASILIANO YALIYOKATIKA YA DARAJA LA GONJA MPIRANI

TANROADS YAANZA KUREJESHA MAWASILIANO YALIYOKATIKA YA DARAJA LA GONJA MPIRANI

 

Kilimanjaro

08 Jan, 2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro umetimiza agizo la Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, la kuhakikisha mawasiliano yaliyokatika kufuatia kuvunjika kwa daraja la Gonja Mpirani baada ya kunyesha mvua kubwa katika safi za milima ya Pare wilayani same mkoani yanarejeshwa haraka.

Daraja hilo, lililopo katika barabara kuu ya Same-Mkomazi, Wilaya ya Same, lilibomoka Januari 2, 2025, baada ya nguzo zake kuathiriwa vibaya na mafuriko, na hivyo kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya kata za Ndungu na Maore.

Kuvunjika kwa daraja hilo kulisababisha usumbufu mkubwa wa usafiri kwa wakazi wa safu za milima ya Upare.

Waziri Ulega, alipotembelea eneo hilo Januari 4, 2025, aliagiza TANROADS kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika kwa haraka.

Alisema, "Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenituma niwape pole kwa changamoto iliyotokea na niwahakikishie kuwa daraja jipya litakuwa tayari haraka ili wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida."

Waziri huyo aliwataka wataalam wa TANROADS kushirikiana na kwa kufanya kazi usiku na mchana. Pia aliwakumbusha mameneja wa TANROADS kote nchini kuchukua tahadhari ya msimu wa mvua, ili kuepusha athari kama hizo.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando, jana siku ya Jumatano Januari 08, 2025 alithibitisha kuwa, ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 95.

Daraja la Gonja Mpirani, lililoko kilomita 55 kutoka Same, ni kiunganishi muhimu kati ya kata za Ndungu na Maore, na ni kiungo muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa eneo hilo