News

MTENDAJI MKUU WA TANROADS AHIMIZA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA MKOA WA MANYARA

MTENDAJI MKUU WA TANROADS AHIMIZA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA MKOA WA MANYARA

Manyara

07 Jan, 2025

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta tarehe 07 Januari, 2025 alitembelea ofisi za TANROADS Mkoa wa Manyara na kufanya kikao na watumishi wa taasisi hiyo.

Katika hotuba yake kwa watumishi, Mtendaji Mkuu huyo amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, nidhamu, na utendaji kazi wa kiwango cha juu kwa wahandisi pamoja na wafanyakazi wote.

Alieleza kuwa uwajibikaji ni nguzo muhimu katika kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja, ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, katika kuelekea kipindi cha mvua, Mhandisi Besta alitoa muongozo wa kiutendaji, akiwataka wahandisi kuchukua tahadhari na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

"Ni muhimu kuhakikisha barabara na madaraja yanapitika wakati wote ili kupunguza kero kwa watumiaji," alisisitiza.

Vilevile, alihimiza watumishi kufanya kazi kwa bidii na weledi, akieleza kuwa juhudi zao ni sehemu ya mafanikio ya TANROADS katika kuhudumia jamii.