News

MIRADI YA DHARURA IFANYIKE USIKU NA MCHANA: MHA. KASEKENYA

MIRADI YA DHARURA IFANYIKE USIKU NA MCHANA: MHA. KASEKENYA

Katavi

09 Jan, 2025

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amewataka wakandarasi wote nchini waliopewa kazi za ujenzi wa miradi ya dharura kufanya kazi usiku na mchana.

 

Mha. Kasekenya, ameyasema hayo tarehe 9 Januari, 2025 mkoani Katavi wakati akikagua miradi ya barabara na madaraja ambayo yaliathiriwa na mvua za El-nino za mwaka 2024.

 

“Miradi hii ni miradi ya dharura na mwaka uliopita mvua iliharibu sana miundombinu ya barabara hasa madaraja na Serikali ilitafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kufanya marejesho ya muda na kuja kujenga madaraja ya kudumu kwa ubora unaoitajika hivyo wakandarasi mhakikishe mnafanya kazi muda wote”, amesema Mha. Kasekenya.

 

Vilevile, Mha. Kasekenya amewasisitiza Wakandarasi pamoja na Kitengo cha Usimamizi wa miradi cha TANROADS (TECU) kusimamia kwa karibu miradi hii kwa kufanya kazi usiku na mchana ili iweze kukamilika ndani ya muda wa miezi 12 kama ilivyopangwa kwa ubora mzuri.

 

Mha. Kasekenya amewataka TANROADS kuwawezesha wakandarasi wazawa katika kufanya kazi kwa weledi kwa sababu wameaminiwa na waoneshe nia kuwa wanaweza kufanya kazi kubwa zaidi.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Katavi Mha. Martin Mwakabende amesema kukamilika kwa madaraja hayo kutatatua changamoto za usafiri katika kipindi chote cha mwaka mzima.

 

Madaraja hayo ni daraja la Katuma-Sitalike, Mirumba-Kitumba pamoja na Daraja la Kilida ambayo yanajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.