News

BARABARA YA MIANZINI-NGARAMTONI KM 18 KUKAMILIKA SEPTEMBA

BARABARA YA MIANZINI-NGARAMTONI KM 18 KUKAMILIKA SEPTEMBA

 

Arusha

06 Januari, 2025

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemtaka Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald Massawe kumsimamia kikamilifu mkandarasi Stecol Corporation anaejenga barabara ya Mianzini-Ngaramtoni Km 18 kuhakikisha inakamilika ifikapo Septemba mwaka 2025.

 

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo amesisitiza kufanyakazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike kwa wakati ili kurahisisha usafiri na usafirishaji jijini Arusha.

 

Amesisitiza ujenzi wa barabara katika miji na majiji uendane na uwekaji taa za barabarani  zinazotumia jua (solar power), ili kupendezesha mitaa na kuiwezesha kupitika wakati wa usiku.

 

"Mh.Rais Samia ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara jijini Arusha hivyo hakikisheni kazi inafanywa kwa ubora, hatutakubali barabara iharibike baada ya muda mfupi ", "amesisitiza  Ulega.

 

Aidha, Waziri huyo amemhakikishia mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuwa Serikali itazijenga barabara zote unganishi na wezeshi jijini Arusha ili kupunguza msongamano wa magari na kuendana na maandalizi ya mashindano ya kombe la mataifa ya Africa AFCON 2027.

 

"Tutahakikisha tunaondoa msongamano kwa kuzijenga barabara zote zenye msongamano na zinazounganisha na kiwanja cha mpira", amesema Ulega.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Makonda ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara jijini Arusha nakusisitiza  itachochea ukuaji wa sekta ya utalii  na kukuza uchumi wa watu jijini humo.

 

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta amesema tayari Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo na wamejipanga kuhakikisha miradi ya  barabara na madaraja inayoendelea mkoani Arusha itasimamiwa na inakamilika kwa wakati.