MKAKATI WA KUPUNGUZA MSONGAMANO DAR, ARUSHA WAJA
Dodoma
31 Desemba, 2024
Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itatoa kipaumbele kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma ili kurahisisha usafiri na usafirishaji katika miji inayokua kwa kasi. Miongoni mwa miradi amesema ni barabara za mzunguko katika Jiji la Dodoma ambazo zimefikia asilimia 80 na upanuzi wa Barabara ya Uyole-Ifisi-Songwe Airport jijini Mbeya ambayo imefikia asilimia 20. Mingine ni awamu za tatu na nne za miundombinu ya barabara za mwendo kasi jijini Dar es Salaam. Pia kuanza huduma kwenye awamu ya pili kwa njia ya Mbagala iliyokamilika. “Mapema mwakani, tunatazamia Reli ya SGR ianze kusafirisha mizigo kwa vipande vya Dar es Salaam hadi Dodoma kiasi cha tani milioni moja kwa mwaka, lengo ni kukuza ushoroba wa kibiashara na kimaendeleo unaochochea uzalishaji na ajira kwa wananchi kote inapopita,” amesema. Rais Samia amesema hayo wakati akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania leo Desemba 31, 2024.