MAJALIWA AIPONGEZA WIZARA YA UJENZI NA TANROADS KUREJESHA MAWASILIANO BARABARA KUU MANYARA - SINGIDA
Manyara
20 Desemba, 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameipongeza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kwa kurejesha mawasiliano ya barabara Kuu ya Manyara - Singida ambayo iliathirika Desema 3, 2023 wakati wa maafa ya maporomoko ya tope la mlima Hanang Mkoani Manyara.
TANROADS ilirejesha hali ya miundombinu iliyoathirika kufuatia maporomoko ya tope eneo la Katesh katika wilaya ya Hanang’ kwa kujenga Barabara za Huduma (Service Roads), Kusimika taa za barabarani, Kuweka paving blocks pande zenye maduka, kujenga mitaro ya mawe na zege, kuweka vivuko vya watembea kwa miguu pamoja na ujenzi wa makalavati sita (6).
Akizungumza Desemba 20,2024 wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Nyumba 109 za waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope zilizojengwa katika kitongoji cha Waret, kijiji cha Gidagamowd wilayani Hanang mkoani Manyara Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imefarijika kwa jitihada za zilizofanywa na Wizara kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha miundombinu hiyo inarejea kama ilivyokuwa awali.
“Niwapongeze Wizara ya Ujenzi, nakuona Mheshimiwa Kasekenya upo hapa, mlifanya kazi nzuri na ya kupongezwa kuhakikisha barabara hii inarejea vizuri”, amesema Majaliwa
Katika hafla hiyo Waziri Mkuu Majaliwa amezindua na kukabidhi jumla ya hati za nyumba 109 ambapo Nyumba 73 zimejengwa na Serikali kwa kuputia SUMA JKT, 35 zimejengwa na RED CROSS na moja imejengwa na Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT).
Aidha, mbali na kukabidhi hati, pia amekabidhi majiko 109 ya nishati safi ya kupikia ambayo ni zawadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa waathirika hao.