News

KASEKENYA AAGIZA KASI IONGEZWE UJENZI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA

KASEKENYA AAGIZA KASI IONGEZWE UJENZI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA

 

Shinyanga

18 Desemba, 2024

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya amemuagiza Mkandarasi China Henan International Cooperation (CHICO) anayejenga mradi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kuongeza kasi ili uweze kukamilika ifikapo Aprili 2025.

 

Katika ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga Desemba 18, 2024 Mha. Kasekenya amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo, lakini amesisitiza Mkandarasi huyo kuhakikisha anaongeza kasi na nguvu kazi na kazi ifanyike usiku na mchana ili kufikia lengo kwa mujibu wa mkataba.

 

"Maendeleo ya mradi ni mazuri mpaka sasa, kikubwa fanyeni kazi usiku na mchana, na muongeze wafanyakazi pamoja na vifaa ili kuongeza kasi ya ujenzi, pamoja na jengo la abiria nalo likamilike kwa wakati", amesema Mha. Kasekenya

 

Mha. Kasekenya ameagiza pia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga na Mhandisi Mshauri SMEC kuhakikisha wanamsimamia kwa karibu Mkandarasi huyo, ili ajenga mradi huo kwa viwango na ubora vinavyohitajika

 

Aidha, Mha. Kasekenya amesema kuwa uwanja huo ni muhimu kwani ukikamilika utakuwa kiunganishi muhimu kwa maeneo ya Ukanda wa Ziwa hasa wakazi wa Shinyanga na maeneo jirani.

 

Kwa Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na kuahidi watasimamia mradi huo na kuhakikisha unakamilika na kukabidhiwa kwa wakati kwani kukamilika kwake utaleta maendeleo na kukuza uchumi  Mkoani  Shinyanga.

 

Awali akitoa Taarifa ya mradi huo, Mha. Mshauri kutoka SMEC Gosbert Ruburi, amesema kuwa kazi zinazoendelea kufanyika ni pamoja na ujenzi wa tabaka la lami kwenye eneo la kuingia na kutokea ndege na eneo la maegesho ya ndege pamoja na ujenzi wa jengo la abiria.

 

Aidha, Mha. Ruburi amefafanua kuwa hadi sasa mradi huo umetoa jumla ya ajira 160 ambapo kati ya ajira hizo asilimia 80 ni kwa Watanzania.

 

Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Shinyannga  wenye urefu wa Kilometa 2.2 unafadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo ni moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mkoa huo na mikoa jirani.