WAZIRI ULEGA AONGEA NA MENEJIMENTI NA MAMENEJA WA TANROADS WA MIKOA YOTE
Dodoma
18 Desemba, 2024
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amekutana na Menejimenti na Mameneja wa mikoa yote 26 ya Tanzania Bara wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na kujadili masuala mbalimbali ya utendaji wa kazi wa kimkakati. Kikaohicho kimefayika Jijini Dodoma.
Waziri Ulega amesema ili kukamilisha miradi ya dharura inakamilika sasa kazi zifanyike kwa nyakati zote za usiku na mchana, kwa kuwa ni miradi hiyo inapaswa kushughulikiwa kidharura.
"Fanyeni kazi kwa kasi tena usiku na mchana hususan kwenye miradi ya dharura ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na adha ya miundombinu iliyoharibiwa”, amesema Ulega.
Ulega amewaambia mameneja hao kuwa wanatakiwa waende kwa spidi inayofanana na viwango vya kasi vinavyoonekana wakati Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapopewa majukumu ya utekelezaji na serikali kwa sababu kuna mvua zinakuja na zinaweza kufanya maeneo yaliyoharibika kuharibika zaidi.
Ulega amesema barabara zilizoharibika kwa sababu ya mvua za masika zilizochanganyika na za El Niño zimesababisha usumbufu na kusimamisha shughuli za uchumi na hivyo ni muhimu zikashughulikiwa kwa haraka.
Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, amewataka mameneja hao kufanya kazi kwa kujiamini na kwa weledi mkubwa, ili kuleta tija na ufanisi katika Sekta ya Ujenzi nchini, ambapo itaondoa kero ya miundombinu mibovu kwa wananchi na itachochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aidha, Ulega ametoa rai kwa Mameneja wa Mikoa yote nchini kuhakikisha maeneo yote yenye msongamamo wa magari hususani kwenye majiji na Manispaa yanafanyiwa usanifu yakinifu kwa ufasaha kulingana na mahitaji ya sasa na miaka mingi ijayo na kuratibiwa vizuri ili kupunguza msongamano na kuwawezesha wananchi kufanya kazi zao kwa wakati.
Mkutano wa Dodoma ulikuwa ni wa kwanza kwa Waziri Ulega kukutana na viongozi wa TANROADS tangu ateuliwe kushika wadhifa huo hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan..
Waziri huyo mpya alitumia nafasi hiyo kupongeza wafanyakazi wa wakala hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe Rais Dkt Samia, imekamilisha ujenzi wa barabara zaidi ya Kilometa 1,198 kwa kiwango cha lami.
Waziri Ulega amewahakikishia Mameneja hao kuwa Serikali awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali za Wakandarasi, ili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kasi na kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour ameeleza kuwa TANROADS itaendelea kuhakikisha barabara kuu, za mikoa na madaraja yanajengwa ili kupitika majira yote ya mwaka.
Balozi Aisha amewataka Mameneja wa TANROADS kuboresha usimamizi wa miradi, kulinda hifadhi za barabara pamoja na kupendezesha miji kwa taa za barabarani na utuzaji wa mazingira pembezoni mwa barabara.